Mwanamke wa Kisasa katika Insha za Kifasihi Magazetini: Mtazamo wa Nadharia ya Upalizi
Abstract
Magazeti yana mchango mkubwa katika kuifahamisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yanayoiathiri. Makala yanayochapishwa magazetini huwawilisha ujumbe kutoka kwa waandishi hadi kwa hadhira ya wasomaji kupitia njia mbalimbali kwa nia ya kuathiri mitazamo na mielekeo yao kuhusu masuala ya kijamii. Mbali na matumizi ya lugha ya kawaida, lugha ya kifasihi kutumika katika baadhi ya makala ili kuhamasisha wasomaji. Mojawapo ya makala hayo ni insha za mienendo za ‘Staffroom Diary’ zinazoandikwa na Frankline Muyonga ambaye ni maarufu kwa jina la Mwalimu Andrew katika gazeti la Sunday Nation, Kenya; The Citizen, Tanzania na Daily Monitor, Uganda. Masuala yanayoangaziwa katika makala haya na aghalabu kwa mseto wa lugha ya Kiingereza na Kiswahili kwa mtindo wa ucheshi ni ya kisiasa, kijamii na kitamaduni. Ingawa insha hizi zimekuwa zikichapishwa tangu mwaka 2009, uchunguzi wa kina haujafanywa kuhusu jinsi zinavyowachora wanawake na athari zake kwa mitazamo na mielekeo ya wasomaji kuhusu jinsia hii. Azma kuu ya makala haya ni kubainisha kasumba au usaguzi chanya (positive stereotypes) unaosindikizwa kwa hadhira katika insha hizi kwa misingi ya Nadharia ya Upalizi (Cultivation Theory) iliyoasisiwa na George Garbner (1969). Mtazamo huu huchunguza athari za vyombo vya habari kwa mitazamo ya hadhira yake kuhusu masuala ya kijamii yakiwamo ya jinsia. Umejikita katika wazo kwamba hatimaye watu huja kuamini wanayoyaona, kusikia au kusoma kwenye vyombo hivi kuwa ni fumano la ukweli au uhalisia wa maisha. Uchunguzi wetu umetalii jinsi mwanamke anavyosawiriwa na jinsi makala haya yanavyojenga mitazamo miongoni mwa wasomaji. Nakala teule za makala ya ‘Staffroom Diary’ pamoja na uchunguzi wa maandishi mbalimbali kuhusu mada hii zimetumiwa kama vyanzo vya data ya utafiti huu. Wasomaji wapenzi wa insha hizi watapata ukweli kuhusu nafasi ya mwanamke katika insha hizi mintarafu ya hali halisi. Halikadhalika, watafiti wa Kiswahili watatumia matokeo ya uchunguzi huu kutafitia zaidi vipengele vingine vya insha za kifasihi katika magazeti.
Full Text:
PDFRefbacks
- There are currently no refbacks.