Taarifa kwa Waandishi wa Makala

Usuli  na Mawanda

MULIKA ni jarida la taaluma ya Lugha na Fasihi ya Kiswahili. Jukumu lake kuu ni kukusanya na kusambaza maarifa yanayohusu Lugha na Fasihi ya Kiswahili yaliyokitwa katika utafiti mpevu. Kutokana na mahitaji kwa baadhi ya watumiaji wa Kiswahili katika nyanja nyingine, hivi sasa jarida hili linapokea pia makala yaliyoandikwa kwa Kiswahili lakini yenye maudhui mengine nje ya Lugha na Fasihi ya Kiswahili. MULIKA limeendelea kuwa daraja kati ya watumiaji wa Kiswahili popote walipo, na wataalamu wa Kiswahili katika shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu Afrika ya Mashariki na kwingineko.

 

Uandaaji na Utumaji wa Makala

Jarida linapokea makala yaliyoandikwa kwa Kiswahili TU. Makala yapigwe chapa katika muundo wa Microsoft Word, mistari ikitengwa kwa kipimo cha nafasi ya 1.5 baina ya mstari na mstari na pambizo liwe na upana toshelevu. Ukurasa wa kwanza wa makala uoneshe jina la makala, jina kamili la mwandishi (au waandishi) wa makala (ikiwa ni pamoja na wadhifa wake), anwani na baruapepe yake. Ukurasa wa pili uoneshe jina la makala na ikisiri isiyozidi maneno 250. Makala yawe na ukubwa wa maneno kati ya 4000-8000 na mapitio ya vitabu maneno 800-1200.

 

Upitiaji na Uhariri wa Makala

Makala yoyote kabla ya kuwasilishwa yawe yamepitiwa vema na mwandishi na kufanyiwa uhariri wa kina kuhakikisha kwamba hayana makosa ya kiuandishi na kimaudhui. Mwandishi anapaswa pia kuhakikisha kwamba taarifa zote zilizomo ndani ya makala ni sahihi na vyanzo vya taarifa hizo ni vyenye kuaminika.

 

Urejeleaji

Unapotaja marejeleo kwenye matini, taja jina la mwisho la mwandishi, likifuatiwa katika mabano na tarehe ya chapisho lake na kurasa zilizorejelewa, k.m. Yahya (1983:139). Kwenye orodha ya marejeleo au bibliografia majina ya warejelewa yapangwe kialfabeti. Tanchini na tanmwisho ziwekwe namba na zitumike pale tu inapobidi. Maelezo ya tanmwisho yatolewe kwenye ukurasa wa pekee mwisho wa makala, yaani kabla ya kuorodhesha marejeleo.

 

Majina ya vitabu, majarida na anwani za tasnifu/tazmili viandikwe kwa italiki. Majina ya makala yawekwe ndani ya alama za kufunga na kufungua semi kama inavyoonekana katika mifano ifuatayo:

 

Kitabu

Massamba, D.P.B. (2017) Historia ya Kiswahili: Mtazamo Mpya 100 KK hadi 2000 BK. Dar es Salaam: Kiswahili Development Limited. 

 

 

Sura ya Kitabu

Hamisi, A.M. (2008) “Filosofia za Sera za Lugha”. Katika J.G. Kiango (Mh.) Maendeleo ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI. kur. 78-100. 

 

Makala ya Jarida

Majariwa D. (2021) “Upenyezaji na Ukubalifu wa Mkururo wa Konsonanti katika Fonolojia ya Kiswahili: Mifano katika Maneno Yaliyopokelewa kutoka Kiingereza na Kiarabu”. Mulika, Juz. Na. 40 (1): 1-23.

 

Makala ya Jarida la Mkondoni

Omari, S.  (2019)  “Gender  Representation  in  Simba  and  Yanga’s  Joking  Cartoons  in  Tanzania”. Eastern African Literary and Cultural Studies. Juz. 5(2): 79-93. Inapatikana katika https://doi.org/10.1080/23277408.2019
.1643606
. Ilisomwa  tarehe 12 Juni 2012.

 

Tasnifu/Tazmili Isiyochapishwa

Peterson, R. (2014) Matumizi na Dhima za Lugha katika Mandhari-lugha ya Jiji la Dar es Salaam. Tasinifu ya Uzamivu (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Saalam. 

 

Gazeti

Duwe, E. (2018) “Zijue Sifa za Kufundisha Kiswahili Nje ya Nchi”. Mwananchi. 16 Oktoba 2018. uk. 13.

 

Mifano na Vielelezo ndani ya Makala

Mifano yote, majedwali, michoro, ramani na picha mbalimbali vipangwe kwa uwazi na unadhifu kwenye kila ukurasa kadiri vilivyotumika. Taarifa zote hizo zinapaswa kutumika kwa kuzingatia kanuni za maadili ya kazi ya kitaaluma. Mathalani, ni muhimu kuweka chanzo thabiti cha taarifa inayoingizwa kwenye makala, iwe ni picha, michoro, mifano na vingine vinavyohusiana na hivyo. Kwa ujumla, data zinazotumiwa katika makala ni lazima ziwe thabiti na zenye kuaminika.

 

Udanganyifu wa Kitaaluma

Kunakili maneno, mawazo, michoro, n.k., kutoka vyanzo vingine bila kubainisha vyanzo husika kutafasiriwa kuwa ni udanganyifu wa kitaaluma na hiyo inaweza kuwa miongoni mwa sababu za makala yako kukataliwa. Ikiwa itabainika kuwa makala yaliyochapishwa katika jarida yamekiuka maadili ya kazi za kitaaluma,  taratibu za kisheria zitachukuliwa kulingana na kanuni na miongozo iliyopo.

 

Ridhaa ya Kuchapisha

Ikiwa makala yatakubaliwa, mwandishi wa makala ataandikiwa barua kupewa taarifa hiyo. Mwandishi wa makala atapaswa kuthibitisha kwa maandishi kwamba makala hayo hayajachapishwa wala kutumwa mahali pengine. Taarifa hiyo itachukuliwa kuwa ni idhini ya makala hayo kuchapishwa katika Jarida la MULIKA.