Tofauti za Matumizi ya Lugha katika Miktadha mbalimbali ya Mazungumzo
Abstract
Makala hii inachunguza tofauti za matumizi ya lugha katika miktadha mbalimbali ya mazungumzo. Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi, na kaida mbalimbali za jamii inayohusika (King’ei, 2010). Muktadha wa mazungumzo ni hali au mahali ambapo mazungumzo yanafanyika. Katika muktadha wa mazungumzo, kuna mambo ambayo huathiri matumizi ya lugha na kusababisha tofauti za matumizi ya lugha baina ya muktadha mmoja na mwingine. Data ya makala hii kwa kiasi kikubwa imekusanywa maktabani kwa kupitia maandiko na kwa kiasi fulani uwandani kwa kuchunguza matumizi tofauti ya lugha miongoni mwa wazungumzaji. Uchambuzi na uchanganuzi wa data umeongozwa na nadharia ya Uchanganuzi wa Kimaeneo ya Fishman (1972). Kwa mujibu wa nadharia hii, matumizi ya lugha katika muktadha wa mazungumzo huathiriwa na mambo makuu matatu: (i) mada ya mazungumzo, (ii) uhusiano wa wazungumzaji, na (iii) mahali pa mazungumzo. Kwa ujumla, matumizi ya lugha kwa kuzingatia muktadha wa mazungumzo, huzaa mitindo tofauti ya uzungumzaji ndani ya jamiilugha inayohusika.