Jarida la Kioo cha Lugha linahimiza kuzingatia maadili bora ya uchapishaji na litachukua hatua kali kwa mwandishi yeyote ambaye atakiuka maadili ya uchapishaji. Waandishi wa makala wanapaswa kuwasilisha makala zinazotokana na tafiti zao ili kulinda sifa nzuri ya jarida. Tabia zisizo za kimaadili kama vile kuwasilisha makala hiyohiyo katika majarida tofauti na ubwakuzi wa kitaaluma haziruhusiwi. Miswada ambayo imeshachapishwa au inafikiriwa kuchapishwa na jarida jingine isiwasilishwe. Waandishi wataje kwa usahihi vyanzo vya taarifa wanaponakili au wanaporejelea kazi za watu wengine. Pia, wanapaswa kupata idhini kwa maandishi kutoka vyanzo husika wanapochapisha matini yoyote (kama vile picha, maudhui ya mtandaoni na michoro) ambayo hawana hakimiliki nayo. Kama makala imeandikwa na waandishi zaidi ya mmoja, mwandishi aliyetuma makala ahakikishe kwamba waandishi wenzake wote stahiki wanajumuishwa katika makala na wamekubali makala hiyo iwasilishwe kwa ajili ya kuchapishwa. Jarida lina haki ya kuondoa makala iliyochapishwa kama ikigundulika kwamba imebwakua taarifa au kuwa na aina nyingine ya tabiaovu katika uchapishaji.
ISSN 0856-552 X (nakala ngumu) & ISSN 2546-2210 (mtandaoni)