Chanzo cha Tofauti za Kileksika na Maana zake Tanzania Bara na Visiwani na Athari zake kwa Watumiaji wa Lugha ya Kiswahili

Mary Zacharia Charwi

Abstract


Ikisiri

Makala haya yamechunguza chanzo cha tofauti za kileksika na maana zake kwa baadhi ya maneno Tanzania Bara na Visiwani na athari zake kwa wazungumzaji na wajifunzaji wa lugha ya Kiswahili. Lengo kuu ni kubaini chanzo cha tofauti hizo na athari zake kimatumizi kama zinawaleta watu pamoja au zinaimarisha mipaka baina ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Data za utafiti huu zimepatikana kupitia mbinu mbili: mosi, mapitio ya machapisho: kamusi mbili za lugha ya Kiswahili, yaani Kamusi la Kiswahili Fasaha lililotungwa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) (2010) na Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyotungwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI)[1] (2013), na ya pili ni mbinu ya hojaji. Uchanganuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Maana kama Matumizi ya Ludwig Wittgenstein (1953). Nadharia hii inasisitiza kwamba maana ya kiyambo fulani itapatikana katika matumizi ya kiyambo hicho. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa chanzo cha tofauti za kileksika na maana zake ni sababu za kihistoria, tofauti za kiutamaduni, sababu za leksika mpya kutumika sambamba na ile ya zamani, ukopaji wa maneno, sababu za motisha wa kimatumizi na tofauti za kilahaja na sababu za kiuteuzi za msamiati. Aidha, matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba zipo athari chanya na hasi zinazotokana na tofauti za kileksika na maana zake. Athari hasi ni kama vile kusababisha mkanganyiko wa maana za kileksika na ugumu wa ujifunzaji lugha. Kwa upande mwingine, kuna athari chanya ambazo ni kukuza lugha kwa kuongeza msamiati na kupanua maana ya msamiati. Makala haya yanahitimisha kwamba ingawa kuna tofauti za kileksika na maana zake kati ya Tanzania Bara na Visiwani, tofauti hizi hazijengi wala kuimarisha mipaka kati ya maeneo hayo bali hutambulisha jamii ya watu wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.


[1] TUKI ambayo kwa sasa inajulikana kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).


Full Text:

PDF

Refbacks

  • There are currently no refbacks.