Athari za Mkengeuko wa Ujumi wa Kiafrika katika Hadithi Fupi Andishi za Kiswahili
Abstract
Mkengeuko wa ujumi katika uga wa fasihi hurejelea hali ama ya mwandishi au msomaji kutovutiwa kuandika au kusoma kazi zinazohusu maisha halisi ya tabaka lake au utamaduni wa jamii yake. Badala yake hugeuka na kuvutiwa kuandika au kuzisoma kazi za fasihi za tabaka au jamii zenye utamaduni usioelekeana na wake (Sanga, 2018). Katika makala hii zimechunguzwa baadhi ya hadithi fupi andishi kutoka katika magazeti ya HabariLeo, Nipashe na Mwananchi ya mwaka 2008 hadi 2014, ambazo ni sehemu ya kipindi cha utandawazi. Hadithi fupi andishi za Kiswahili za kipindi hiki cha utandawazi, zimekengeuka kiujumi kutoka kwenye zile za asili ambazo ni hadithi fupi simulizi. Ukengeufu umejikita katika namna hadithi zinavyotungwa, zinavyohifadhiwa, zinavyoifikia hadhira, masuala yanayojadiliwa, mahali na wakati wa kusomwa. Hali hiyo imeufanya utanzu huu kuwa na sifa zinazokaribiana na riwaya kiasi cha kupoteza utambulisho wake. Aidha, hadithi fupi za sasa zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na usasa pamoja na umiji, jambo lililosababisha utanzu huu kuibagua hadhira, kirika na kimaeneo. Vilevile, maudhui ya hadithi fupi andishi yameonekana kuwa na mvuto kwa vijana wa mjini kuliko wazee. Hii ni kwa sababu visa vyake vingi na matukio huhusu mapenzi ya kisasa, masuala ya uhalifu, ugaidi na maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu. Matukio haya yanawagusa zaidi vijana kuliko wazee. Jamii za sasa za Kiafrika zimekengeuka kiujumi na kuvutiwa na mambo yanayofungamana na utamaduni wa Kimagharibi kuliko wa Kiafrika
Full Text:
PDFRefbacks
- There are currently no refbacks.